Nawezaje kufanya vizuri katika maswali ya interview ya kazi?
Jiunge MojaSky ili uweze kuuliza maswali, kujibu maswali ya watu wengine na kutengeneza connection
Login MojaSky ili uweze kuuliza maswali, kujibu maswali ya watu wengine na kutengeneza connection
Umesahau password yako?. Andika email yako hapo chini alafu bonyeza 'Reset'. Utapokea link katika email yako kwa ajili ya kutengeneza password mpya.
Tafadhali elezea kwa nini unahisi chapisho hili linapaswa kuripotiwa
Salim Jumbe
Vijana wengi wenye ufaulu mzuri wanaoomba kazi, hujikuta pasipokujua, wakifanya makosa madogo yanayowagharimu. Kwa kuwa umetumia muda wako kuandika barua, kuandika wasifu wako wa kazi, wakati mwingine kusafiri kwenda kuhudhuria usaili, ni muhimu kufanya maandalizi yatakayokuongezea nafasi ya kufanikiwa.
Katika makala haya, tutaangazia baadhi ya maswali yanayoulizwa kwenye usaili wa kazi na namna unavyoweza kuyajibu.
Mapokezi
Unapokaribishwa kwenye usaili, jambo la kwanza ni kuhakikisha kuwa unatengeneza taswira ya mtu anayejitambua, mkomavu na mwenye nidhamu. Salimia jopo linalokupokea kwa tabasamu na salamu ya adabu yenye kuonesha kujiamini. Ikiwa ni lazima kushikana mikono na wanajopo, fanya hivyo kwa kujiamini.
Unapojibu maswali, epuka kutikisa kichwa. Kukunja nne, kuegemea nyuma, au kuweka mikono kwa namna inayoonesha mamlaka, ni kutuma ujumbe hasi usiokusudiwa.
Utambulisho
Kumbuka kuwa usaili wako ulianza tangu jopo la usaili lilipopokea nyaraka zako. Kwa kiasi fulani, tayari wanayo taswira fulani kukuhusu. Una kazi muhimu ya kuwathibitishia kuwa hayo uliyoyaandika yana ukweli.
Mara nyingi unapokaribishwa kwenye usaili, kiongozi wa jopo la usaili, atawatambulisha kwa wenzake. Anapofanya hivyo, ana lengo la kukufanya uwazoee wanajopo, utulie na usiwe na wasiwasi. Shukuru kwa utambulisho wao.
Kiongozi huyo anaweza kukutambulisha wewe kwa jina lako na kukaribisha maswali. Mara nyingi swali linaloanza ni, ‘Tuambiwe wewe ni nani?’ ‘Karibu ujitambulishe…’
Swali kama hili halihitaji utaje majina yako bali kufahamu mhutasari wako kikazi. Ingawa utakayoyasema yatatokana na uliyoyaandika kwenye wasifu wako wa kazi, mara nyingi hautarajiwi kurudia maelezo hayo.
Ari na uwezo wako wa kazi
Unaweza kuulizwa, ‘Kwa nini unafikiri tukuchukue kwa nafasi hii?’, ‘Kwa nini unataka kufanya kazi na sisi?’ Watu wengi wanapoulizwa swali hili hufikiri wanachohitaji ni kujilinganisha na wengine kwa majina. Huna sababu ya kuwataja wengine kama namna ya kuonesha unavyofaa zaidi.
Kwa swali kama hilo, kimsingi wanataka kuona kama unaielewa taasisi yao. Thibitisha kuwa umeitafiti taasisi kwa kina, na una uelewa wa huduma wanazotoa. Onesha unavyojisikia kuwa sehemu ya malengo mapana ya taasisi yao.
Uzoefu wako huko ulikotoka
Unaweza kuulizwa maswali mengi kuhusu uzoefu wako kazini. Ikiwa kwenye wasifu wako wa kazi ulionesha kuwa uliwahi kufanya kazi mahali na ukaiacha, unaweza kuulizwa swali, ‘Kwa nini uliacha kazi yako?’ au ‘Kwa nini unataka kuacha kazi uliyonayo?’
Hili ni swali gumu. Mwuulizaji analenga kupima uaminifu wako na anataka kujua mambo gani hasa yanakuridhisha kazini. Kimsingi lengo sio kujua yaliyofanyika huko uliko (kuwa) bali kujua unavyoweza kumfaa. Hutakiwi kuzunguka kwa kutafuta sababu zisizo za kweli. Jibu kwa urahisi na uwazi lakini ukiwa makini.
Matarajio yako kwa mwajiri
‘Unadhani tukulipe mshahara kiasi gani?’
Hili swali linatafuta kujua vipaumbele vyako uwapo kazini. Ni kweli unatafuta kazi ili upate fedha uboreshe maisha yako. Lakini kuonesha kuwa ari na kujituma kwako kazini kunategemea na kiasi cha pesa unacholipwa ni kosa la kiufundi. Kosa hili linaweza kuwa kikwazo cha kukupa kazi.
Unahitaji kuonesha ukomavu kwa kuelewa kuwa taasisi bora [kama hiyo unayotaka ikuajiri] zina utaratibu rasmi wa kuwalipa wafanyakazi wake. Mtu hulipwa kwa sifa alizonazo. Kwa uelewa huo, utapata alama za ziada.
Uelewa wa mambo na ujuzi wa kazi
Unaweza kuulizwa maswali yanayopima uelewa wako wa kawaida kwa mambo yanayofahamika. Lakini pia unaweza kuulizwa masuala ya moja kwa moja yanayohusiana na kazi unayoomba.
Wakati mwingine, baadhi ya wasaili hutumia mtihani wa kuandika kujaribu kuthibitisha kama kweli una uwezo na ujuzi uliouonesha kwenye wasifu wa kazi.
Malengo yako ya baadae
‘Unajiona ukifanya nini baada ya miaka 10 ijayo?’
‘Una malengo gani ndani ya miaka mitano ijayo?’
Hapa unahitajika kuonesha ari ya kukua kiujuzi na kiweledi. Ongelea mipango ya kujifunza zaidi kufikia kwenye malengo makubwa yanayoendana na malengo mapana ya kitaasisi. Kuzungumzia malengo yasiyoendana na kazi unayoomba kutakupunguzia alama.
‘Umeomba kazi kwingine?’
Wanahitaji kuwa na uhakika na maamuzi yako. Ni kweli inawezekana utakuwa umeomba kazi maeneo mengine. Lakini utaonekana mkomavu ukiweza kuonesha kuwa kazi hii unayosailiwa ndio chaguo la kwanza.
‘Utafanya kazi na sisi kwa muda gani?’
Hapa wanataka kujua kama wewe ni mpitaji au la. Inawezekana kweli unaweza kuwa na mpango wa kufanya kazi kwa muda mfupi na utafute njia nyingine.
Lakini kuonesha wazi kuwa unapita wakati hata kazi hujapata si busara. Onesha ungependa kufanya kazi kwa muda mrefu kadri utakavyohitajika.
‘Unaota kufanya kazi gani nzuri baadae?’
Ukitaja kazi nyingine mbali na hiyo unayoomba, unaleta wasiwasi kuwa hutaridhika na kazi unayoomba. Ongelea mazingira ya kazi bila kutaja kazi mahususi. Mfano, kazi inayokufanya utumie vipaji vyako na ujuzi ulionao. Kazi inayokufanya ukue kiujuzi na kiuzoefu.
Fursa ya kuuliza swali
Kwa kawaida, baada ya kuulizwa maswali mengi, kikao cha usaili kitahitimishwa kwa kukukaribisha kuuliza swali. Kama tulivyosema, kila swali lina maana. Unapoulizwa, ‘Je, una swali ungependa kuuliza?’ lengo ni kutaka kujua ulivyo na ari ya kufanya kazi na taasisi hiyo
Usipouliza swali lolote, maana yake ama huna uelewa wa mambo mengi au huna ari ya kutosha. Uliza swali kuhusu taasisi hiyo. Waliuze wanatarajia nini kwa mtu atakaye pata kazi hiyo. Kadhalika, waweza kuulizia mambo yanayohusiana na fursa wanazoweza kutoa kukuza ujuzi wako kama mfanyakazi wao.
Izo ni baadhi ya Aya tu Kwa urefu zaidi soma Hapa